Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John
Pombe amewaagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi.
Isack Kamwelwe na Mtendaji Mkuu wa TANROADS kusimamia Ujenzi wa Daraja la
Mto Sibiti linalounganisha mikoa ya Simiyu na Singida na kuhakikisha
linakamilika ifikapo Machi, 2019.
Rais Magufuli ameyasema hayo Septemba 10, wakati
akizungumza na wananchi wa mikoa ya Simiyu na Singida katika Kijiji cha Nyahaa
wilayani Mkalama Mkoani Singida muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi
ujenzi wa daraja hilo.
Amesema daraja hilo limeanza kujengwa muda mrefu na
akazikataa sababu zilizotolewa na Mkandarasi kuwa zimepelekea kuchelewesha
ukamilishaji ikiwemo mkandarasi kufanya kazi miezi minne tu kwa mwaka kutokana
na eneo hilo kuwa na maji mengi hususani kipindi cha mvua.
"Wananchi wa hapa wanahitaji daraja limalizike
hawahitaji sababu, mkandarasi alipokuwa akiomba kazi hakujua kuwa hapa maji
huwa yanapita, ma-engineer hawakujua? Hapa hakuna sababu,msitafute
kisingizio"
"Mhe. Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote,
Mtendaji Mkuu TANROADS nataka daraja hili sasa likamilike, mimekuja kwa
makusudi kuweka jiwe la msingi nataka siku nikirudi nipite juu" alisema
Rais Magufuli
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi. Isack Kamwelwe amesema Daraja la Mto Sibiti likikamilika
litakuwa mkombozi katika kuunganisha mikoa ya Kanda ya Ziwa na mkoa wa Singida
na kuahidi ujenzi wa kilomita 25 za lami kwenye tuta la daraja hilo.
"Daraja hili limejengwa katika viwango vya juu
sana, tuta lake pia limejengwa kwa kiwango cha juu sana na tayari tumeshaongea
na TANROADS kwamba kupitia kwenye fedha za matengenezo, tuta hili kwa karibu
kilomita 25 tutaziweka lami Mhe. Rais, tutaposhindwa tutakupa taarifa"
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi. Patrick
Mfugale amesema kazi ya Ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti inayofanywa na Mkandarasi
Hainan
International Limited kutoka nchini China na mpaka sasa umefikia asilimia 70 na hadi
kukamilika kwake litagharimu jumla ya shilingi bilioni 16.3.
Rais amehitimisha Ziara yake ya siku tatu mkoani
Simiyu Septemba 10, ambapo akiwa Simiyu alipata nafasi ya kuweka mawe ya
msingi, kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi
katika maeneo mbalimbali kupitia mikutano ya hadhara.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment