Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka amezindua kampeni ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL) Rudi Nyumbani
Kumenoga mkoani humo na kuipongeza TCCL kwa kuboresha huduma zake na
kuwa miongoni mwa mashirika ya Serikali yanayotoa gawio kwa Serikali, fedha
ambazo zinasaidia kuboresha huduma za jamii na miundombinu.
Akizindua kampeni hiyo jana jioni Septemba 21, 2018 Mjini
Bariadi, amesema kwa mara ya kwanza TTCL imetoa gawio kwa serikali fedha ambazo
sehemu zimewezesha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ulioanza na Jengo la
Wagonjwa wa nje (OPD), ujenzi wa Barabara, miundombinu mingine pamoja na huduma
mbalimbali kwa jamii.
Aidha, Mtaka ametoa wito kwa
wananchi kutumia huduma za TTCL na kumuomba Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Bw.
Waziri Kindamba kufungua ofisi mkoani Simiyu, kumleta meneja na kuongeza
watumishi ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma.
Ameongeza kuwa Mtendaji Mkuu wa TTCL aimarishe mfumo wa
intaneti zaidi ili kuwezesha mpango wa mkoa wa Simiyu wa kufundisha kupitia
teknolojia ambapo mtandao wa intaneti utahitajika kwa kiasi kikubwa.
“Tungehitaji tuone wanafunzi wa
Simiyu wasome saa 24, wanafunzi wasio na walimu wa kutosha wa sayansi tutajenga
vyumba vya madarasa vitakavyowezesha wao kusoma kupitia mfumo wa teknolojia, Mtendaji
Mkuu wa TTCL imarisha mtandao wa TTCL wanafunzi wapate intaneti ili tuweze
kurahisisha ufundishaji kwenye miji mikuu ya wilaya zetu” alisema.
Wakitoa maoni yao huduma za TTCL baadhi
ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu wamesema walikuwa hawazitumii lakini baada ya
shirika hilo kuboresha huduma zake hasa za mtandao wa intaneti wameanza
kuzitumia na wakaomba ziendelee kuboreshwa zaidi.
“ Mimi nilikuwa sijawahi kutumia
mtandao wa TTCL nilikuwa natumia mitandao mingine tu lakini nilivyoona
matangazo nikasema ngoja nijaribu, nikaenda kununua laini na kuanza kutumia,
napenda kutumia zaidi intaneti yao iko
vizuri” alisema Emmanuel Elias mkazi wa Bariadi
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Bw.
Waziri Kindamba ametoa wito kwa Watanzania wote kurudi nyumbani na kuendelea
kutumia huduma za TTCL kwa kuwa kadri wanavyotumia huduma hizo wanazalisha
faida ambayo itaendelea kutumika hapa nchini kwa maendeleo ya nwananchi na
Taifa kwa ujumla.
Aidha, kutokana na Taarifa ya kuwa
na siku nne za maombolezo kwa Taifa ililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kufuatia ajali ya Kivuko cha MV Nyerere
huko Ukerewe Mkoani Mwanza, Mkurugenzi Kindamba amesema TTCL haitaendelea na
kampeni hiyo RUDI NYUMBANI KUMENOGA mpaka siku hizo zipite ili kuungana na
Watanzania wengine kuomboleza juu ya msiba huu wa Taifa.
“Mhe. Rais ametangaza siku nne za
maombolezo kuanzia tarehe 21 Septemba hadi Septemba 24, 2018 kufuatia ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV
Nyerere, tulikuwa tumepanga kuanza na Simiyu, twende Kahama halafu Tabora
lakini kwa sababu ya msiba huu uliotugusa Watanzania wote na kwa kuwa Shirika hili ni la Watanzania na sisi tumeguswa
hivyo itabidi shughuli hii tuisitishe kwa muda; Mungu awarehemu wenzetu
waliotangulia na majeruhi wapone haraka” alisema.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mkoa huo pamoja na baaadhi ya
Viongozi wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) katika Uzinduzi wa Kampeni ya Rudi
Nyumbani Kumenoga uliofanyika Mjini Bariadi jioni ya Septemba 21, 2018.
Kutoka kushoto Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mtendajii
Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Kindamba na Mkuu wa Wilaya ya itilima, Mhe. Benson
Kilangiwakifurahia jambo wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Rudi Nyumbani
Kumenoga uliofanyika Mjini Bariadi jioni ya Septemba 21, 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka(kulia)akimweleza jambo Mtendajii Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Kindamba katika
Uzinduzi wa Kampeni ya Rudi Nyumbani Kumenoga mkoani Simiyu uliofanyika Mjini
Bariadi jioni ya Septemba 21, 2018.
Mtendajii Mkuu wa TTCL Bw. Waziri
Kindamba(aliyenyosha mkono) akitambulisha rasmi Kampeni ya Rudi Nyumbani
Kumenoga kwa wananchi wa mkoa wa Simiyu. katika Uzinduzi wa Kampeni hiyo
uliofanyika Mjini Bariadi jioni ya Septemba 21, 2018.
Baadhi ya wananchi wa Mji wa Bariadi
mkoani Simiyu walioshiriki katika Uzinduzi wa Kampeni ya Rudi Nyumbani Kumenoga
uliofanyika Mjini Bariadi jioni ya Septemba 21, 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka akizindua Kampeni ya Rudi Nyumbani Kumenoga ya TTCL Mjini Bariadi, jioni
ya Septemba 21, 2018.
Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Aslay
akitoa burudani kwa wananchi wa Mji wa Bariadi mkoani Simiyu walioshiriki katika
Uzinduzi wa Kampeni ya Rudi Nyumbani Kumenoga uliofanyika Mjini Bariadi jioni
ya Septemba 21, 2018.
Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Shilole
akitoa burudani kwa wananchi wa Mji wa Bariadi mkoani Simiyu walioshiriki katika
Uzinduzi wa Kampeni ya Rudi Nyumbani Kumenoga uliofanyika Mjini Bariadi jioni
ya Septemba 21, 2018.
0 comments:
Post a Comment