Vifo vya Watoto Wachanga
mkoani Simiyu vimepungua kutokana na Serikali kutoa elimu ya uzazi na wazazi
kuanza kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye semina ya
Mkunga Okoa Maisha iliyofanyika mwishoni mwa wiki jana mjini Bariadi, Katibu wa
Wakunga mkoani humo Daud Marwa alisema vifo vimepungua kutokana na jamii kuanza
kujenga tabia ya kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya.
Alisema kwa mkoa wa Simiyu mwaka 2016 walizaliwa
watoto 47,193 lakini waliokufa walikuwa 655, mwaka 2017 walizaliwa watoto
38,442 na walikufa watoto 617 huku mwaka huu wamezaliwa watoto 37,098 na hadi Septemba
wamefariki watoto 290.
“Vifo vya Watoto Wachanga
mkoani Simiyu vimepungua kutoka 617 mwaka 2017 na kufikia 290 hadi mwezi
septemba mwaka huu kutokana serikali kutoa elimu ya uzazi na wazazi kuanza
kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya, hii ni jitihada kubwa
sana kwani wakunga wamekuwa wakipatiwa mafunzo mara kwa mara, pia kuongezewa
stadi za kumhudumia mama na mtoto mwenye uhitaji pindi anapozaliwa’’ alisema
Marwa.
Aliongeza kuwa timu ya watumishi wa afya inaendelea
kufanya ufuatiliaji na usimamizi ili kuhakikisha kila mama mjamzito anajifungua
salama na mtoto mchanga anaendelea kuishi akiwa salama.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Mkunga Okoa Maisha
Martha Rimoy alisema akinamama wajawazito wengi wao wanapoteza maisha kutokana
na kutoka damu nyingi kabla ya kujifungua, wakati wa kujifungua na baada ya
kujifungua.
Alisema wanawake 556 kati ya vizazi hai 100,000
hufariki dunia kila mwaka kutokana na kutokwa damu wakati wa kujifungua na
kifafa cha mimba, uzazi pingamizi, na uambukizo.
Aliongeza kuwa kutokana na takwimu hizo, hali ya vifo
vya wakinamama na watoto wachanga bado ni mbaya sana hivyo serikali,
wadau wa maendeleo na wananchi wanatakiwa kupiga vita vifo hivyo.
Aidha, katibu
huyo alisema baadhi ya wanawake mkoani Simiyu bado wanajifungulia majumbani
kutokana na kuwepo kwa wakunga wa jadi na akabainisha kuwa wanaendelea kutoa
elimu kwa wakina mama ili waache tabia hiyo badala yake wajifungulie katika
vituo vya kutolea huduma za afya ili kuepuka vifo vinavyoweza kuzuilika.
‘’Tunaendelea kutoa elimu kwa wakunga wa jadi na
wakinamama wajawazito ili wakipata matatizo ambayo yanazuilika waweze kuwahi
vituo vya kutolea huduma za afya, kutoa mafunzo kwa watoa huduma na pia
kuboresha sehemu za kutolea huduma’’ alisema Martha Rimoyi.
Naye Katibu Mkuu wa chama cha Wakunga nchini ambaye
pia ni Mwalimu wa Wakunga chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi (MUHAS) Dkt.
Sebalda Leshabari alisema kazi ya mkunga ni kumshauri mama mjamzito juu ya
masuala ya uzazi hadi anapojifungua, lakini kazi ya muuguzi ni kuhudumia
mgonjwa.
Alisema wakunga ni watu wenye taaluma ya ukunga na
wenye stadi za kuhudumia mama mjamzito, wenye kugundua viashiria vya hatari kwa
wajawazito na kutoa rufaa tofauti na wakunga wa jadi ambao hawana taaluma
yoyote.
‘’Wakunga wa jadi hawana stadi na utaalamu pindi mama
mjamzito anapokuwa na dalili za kushindwa kujifungua salama, hivyo tunawaomba
wakinamama wajawazito wajenge tabia ya kujifungulia kwenye vituo vya kutolea
huduma ya afya ili kuzuiwa vifo visivyokuwa vya lazima’’ alisema Dkt.
Leshabari.
Semina hiyo ya siku moja kwa waandishi wa Habari mkoa
wa Simiyu ililenga kuwajengea uelewa na kufahamu juu ya mkunga, muuguzi na
mkunga wa jadi kupitia mradi wa Mkunga Okoa Maisha unaolenga kupunguza vifo vya
akinamama wajawazito na watoto wachanga.
MWISHO.
Katibu wa Chama cha
Wakunga Tanzania, Dkt. Sebalda Leshabari akizungumza na
waandishi wa habari wa mkoa wa Simiyu katika semina ya Mkunga Okoa Maisha
iliyofanyika mwishoni mwa wiki jana mjini Bariadi.
Mratibu wa Mradi wa
Mkunga Okoa Maisha Martha Rimoy akizungumza na waandishi wa habari wa mkoa wa
Simiyu katika semina ya Mkunga Okoa Maisha iliyofanyika mwishoni mwa wiki jana
mjini Bariadi.
Katibu wa Wakunga mkoani
Simiyu Daud Marwa(kulia) na baadhi ya waandishi wa habari wa mkoa wa Simiyu
wakimsikiliza Katibu wa Chama cha Wakunga Tanzania, Dkt. Sebalda Leshabari katika semina ya Mkunga Okoa Maisha iliyofanyika
mwishoni mwa wiki jana mjini Bariadi.
Baadhi ya waandishi wa
habari wa mkoa wa Simiyu wakifuatlia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika
semina ya Mkunga Okoa Maisha iliyofanyika mwishoni mwa wiki jana mjini Bariadi.
Baadhi ya waandishi wa
habari wa mkoa wa Simiyu wakifuatlia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika
semina ya Mkunga Okoa Maisha iliyofanyika mwishoni mwa wiki jana mjini Bariadi.
Baadhi ya waandishi wa
habari wa mkoa wa Simiyu wakifuatlia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika
semina ya Mkunga Okoa Maisha iliyofanyika mwishoni mwa wiki jana mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment